Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania – TEF, Deodatus Balile amesema, wadau wa habari wangependa ukamilifu wa uundwaji wa kanuni za habari usivuke mwezi Oktoba 2023.
Balile ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na baadhi ya wanahabari katika ofisi za jukwaa hilo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mwenye jukumu la kusimamia na kukamilika kwa kanuni ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Amesema, “Tungependa kanuni za habari zipatekane mpaka kufika Oktoba, hili ni ombi kwa kuwa, Waziri wa Habari (Nape Nnauye) halazimishwi na sheria kuhusisha wadau, ni kutokana na utaratibu wake wa kushirikisha wadau ndio maana anafanya hivyo, wala safari hii suala la kanuni za habari halipelekwi bungeni, linaishia kwa kwake Waziri Nape.”
Balile ameongeza kuwa, baada ya bunge kupitisha marekebisho ya sheria ya habari, kinachofuata sasa ni kuomba fursa ya kukutana na serikali kwa ajili ya kupendekeza mambo gani yaingie kwenye kanuni.
Aidha amesema miongoni mwa mambo ambayo wadau wa habari wangependa kuona yanaingia kwenye kanuni mpya na kuanza kutumika ni pamoja na suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano tofauti na ilivyo sasa.
Kwenye mkutano wake na wanahabari, Balile alisema, eneo lingine wanalotarajia liingie kwenye kanuni, ni umiliki wa hisa katika vyombo vya habari kutowekewa mipaka.