Serikali inatarajia kuwa na mashamba darasa kumi kila wilaya hapa nchini kwa ajili ya kutambulisha teknolojia mpya ya malisho ya mifugo ijulikanayo kama JUNCAO kutoka nchini China ili kukabiliana na uhaba wa malisho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 8, 2022 katika warsha iliyowahusisha wadau wa mifugo kutoka sekta binafsi na umma, taasisi na mashirika kutoka ndani na nje ya nchi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesema katika uanzishaji wa mashamba hayo kutaanza na utoaji wa elimu kwa wadau kupitia semina mbalimbali ili waweze kufahamu teknolojia hiyo na kulima malisho hayo ambayo yanastahimili ukame.

Aidha, ameongeza kuwa uwepo wa teknolojia ya malisho hayo ambayo yamefanyiwa utafiti katika baadhi ya mashamba ya malisho ya serikali yameonesha kutoa matokeo mazuri kwa kuwa na virutubisho muhimu kwa mifugo na yanastawi kwa wingi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Asimwe Rweguza, amesema lengo kuu la warsha iliyofanyika leo ni kujadili na kupata uzoefu juu ya teknolojia mpya ya malisho aina ya JUNCAO pamoja na uzalishaji wa uyoga ili kuzalisha kwa wingi malisho na uyoga na kuboresha mifugo iliyopo.

Dkt. Rweguza amebainisha kuwa JUNCAO ni teknolojia ya malisho aina ya nyasi zinazotumika kwa ajili ya mifugo na kwamba malisho hayo yamefanyiwa utafiti nchini China na kuonekana yanakuwa haraka na yana kiwango kikubwa cha protini na shina moja la JUNCAO linatoa matawi mengi.Katika warsha iliyofunguliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, juu ya teknolojia mpya ya malisho aina ya JUNCAO kutoka nchini China inaelezwa kuwa na lengo kuu la kuhakikisha teknolojia hiyo inapunguza uhaba wa malisho kwa ajili ya mifugo hususan wakati wa ukame.

Mzee Hassan Dalali apata ajali
Mbowe aeleza sababu zilizomkutanisha na Rais Samia