Tume ya Utangazaji Zanzibar imekifungia kituo cha televisheni cha Tifu kwa muda wa siku saba kwa kosa la kurusha vipindi vinavyokwenda kinyume na uombolezaji wa msiba wa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Omar Said amesema kuwa baada ya Rais wa Zanzibar kutangaza maombolezo, tume ilitoa muongozo wa urushaji matangazo na vipindi kwa siku saba za maombolezo kwa televisheni, Redio na mitandao ya kijamii.
Aidha katika muongozo huo, tume imevitaka vituo vyote kubadilisha ratiba zao za urushaji wa matangazo na vipindi, na kuandaa vipindi maalum vya maombolezo katika muda huu wa siku saba, huku ikiweka wazi kwamba haitakuwa tayari kuona kuna kituo kinakwenda kinyume na mwongozo huo.
Said amesema licha ya hatua hiyo ya kutoa mwongozo kwa vituo hivyo, lakini kituo cha Tifu kimeonekana kwenda kinyume na muongozo huo, hivyo ililazimika kuchukuliwa hatua hiyo, ili kutoa fundisho juu ya kufuata muongozo wa serikali katika urushaji na uandaaji wa vipindi.
Aidha, Said ameviomba vyombo vya habari kufuata kikamilifu muongozo uliotolewa na Serikali kupitia Tume ya Utangazaji juu ya urushaji wa vipindi na utangazaji katika kipindi hiki cha msiba wa Maalim Seif aliyefariki jana wakati akipatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.