Mlinda mlango wa kutumainiwa katika timu ya taifa ya Hispania David de Gea, amekiri kutokufurahishwa na mpira utakaotumika wakati wa fainali za kombe la dunia za 2018, zitakazounguruma nchini Urusi kuanzia Juni 14.
Mlinda mlango huyo ambaye pia ni chaguo la kwanza katika kikosi cha Man Utd , ameweka wazi kauli ya kutoufurahia mpira huo (Telstar 18 ball), baada ya kutumika katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita, na kushuhudia timu hizo zilienda sare ya kufungana bao moja kwa moja.
Akizungumza na gazeti la AS Spanish (Spanish newspaper AS), De Gea amesema mpira huo ni mgeni katika mikono yake na ulimpa wakati mgumu kuumudu ulipofika katika himaya ya lango la Hispania wakati wa mchezo dhidi ya Ujerumani.
“Una mazingira magumu, na ulikua mgeni sana kwangu, hivyo sijaufurahia kwa sababu ninaamini itanichukua muda kuuzoea.” Amesema De Gea
Hata hivyo De Gea sio mlinda mlango wa kwanza kulalamikia mpira huo, bali kipa mwingine kutoka Hispania Pepe Reina, amekua sehemu ya watu waliolalamika.
“Ni kama mtu unabahatisha kuutumia, nimejaribu kuuzoea nilipokua mazoezini lakini bado ni mgumu kuzoeleka, itakua ni vigumu kwa walinda milango wengine kuuzoea kwa sababu una mazingira tofauti na ilivyo mipira mingine tunayoitumia katika ligi.” Amesema Reina.