Mnyama aina ya Ndovu au Tembo wa Mbuga ya Kitaifa ya Samburu nchini Kenya, amejifungua ndama pacha katika kile ambacho shirika la ‘Save the Elephants Kenya’ ilitaja kuwa tukio la kusisimua na nadra kutokea.
Shirika hilo kupitia mitandao ya kijamii liliripoti kwamba mama ndovu kwa jina la Bora kutoka Winds Family alijifungua ndama wa kiume na wa kike mwishini mwa wiki iliyopita ambapo wahudumu katika kambi ya Ndovu waliwaona pacha hao katika Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu na kuwaarifu watafiti wa Save the Elephants
“Kuzaa pacha ni nadra sana – kwa kweli, hili ni jambo la kushangaza ambalo hatujaona pacha katika bustani kwa miongo kadhaa, tutahakikisha kuwa tunakufahamisha kuhusu jinsi malaika hawa wadogo wanaendelea,” Shirika la Save the Elephants ilichapisha mnamo Jumanne, Januari 18.
Waziri wa Utalii, Najib Balala, alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kutoa maoni yao kuhusu tukio hilo. “Hongera! kwa Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu kwa kuzaliwa kwa ndama pacha wa ndovu,” ujumbe wake ulisema katika mtandao wake wa Twitter.
Kulingana na Spana, shirika linalojishughulisha na ustawi wa wanyama, ndovu huwa na mtoto mmoja tu kwa wakati mmoja. Hata hivyo, kuna matukio ambapo ndovu wanaweza kupata pacha, lakini hii hutokea tu katika 1% ambayo ni ndogo ikilinganishwa na wanadamu, ambapo 1.6% ya kuzaliwa ni pacha.
Tembo wa Kiafrika hubeba mimba hadi miezi 22, wakati tembo wa Asia huwa na mimba kwa miezi 18-22 na hiki ndicho kipindi kirefu zaidi cha ujauzito kati ya mamalia wote, ambayo inaleta maana tunapofikiria jinsi tembo walivyo wakubwa.
Mnamo Septemba 2021, ndovu mmoja huko Sri Lanka alijifungua ndama pacha katika kituo cha watoto yatima cha Sri Lanka, ambapo ilikuwa mara ya kwanza nchini humo katika miaka 80.