Meneja wa Kikosi cha Manchester United Ten Hag ameunga mkono mpango wa Klabu hiyo kuingizwa Sokoni na wamiliki wa sasa Familia ya Glazer, kwa kusema litakua jambo bora zaidi kwa maslahi ya Klabu.
Familia ya Glazer ambayo ni magwiji wa Biashara nchini Marekani, waliinunua Klabu ya Manchester United mwaka 2005 kwa thamani ya Pauni Milioni 790 sawa na Dola Bilioni 1.34.
Hag ambaye aliajiriwa Klabuni hapo Mwanzoni mwa msimu huu akitokea Ajax Amsterdam ya nchini kwao Uholanzi, amesema endapo Biashara itafanyika na Klabu hiyo kuwa chini na Mwekezaji upya, kutakua na kila sababu ya kupiga hatua ndani na nje ya Uwanja.
“Kutakuwa na uwekezaji zaidi unaowezekana ambao ni mzuri,”
“Uongozi umenihakikishia kuwa Biashara ya kuuzwa kwa klabu ikifanyika, hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya kitamaduni na uendeshaji, hivyo Manchester United itaendelea kuwa na utamaduni wake,”
“Itakuwa bora zaidi kwa sababu pesa nyingi zitapatikana kwa kuiwezesha klabu hii kupiga hatua kubwa, binafsi ninapenda iwe hivyo kwa sababu tunataka kuona mambo yakisogea kwa haraka zaidi.” amesema Ten Hag
Hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu mnunuzi mpya wa Klabu ya Manchester United, licha ya baadhi ya Matajiri wakubwa kuanza kutajwa katika harakati za kuwania nafasi kumiliki Klabu hiyo nguli Barani Ulaya.