Aliyekua nahodha wa timu ya taifa ya England Terry Butcher kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 1980–1990, amejiuzulu kukifundisha kikosi cha timu ya taifa ya ufilipino (Philippines), kabla ya kuanza kufanya kazi rasmi.

Butcher alitangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa hilo inayotambulika kwa jina la utani Azkals (Street Dogs), akichukua nafasi ya Thomas Dooley mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu, na alitarajiwa kuanza kazi mapema mwezi ujao.

Dhumuni kubwa la kocha huyo kuajiriwa na chama cha soka nchini Ufilipino, lilikua ni kuiwezesha timu ya taifa hilo kushiriki kwa ushindani katika fainali za bara la Asia ambazo zitaunguruma Falme Za Kiarabu kuanzia Januari 05 mwaka 2019.

“Ninaomba radhi kwa kutangaza kuwa, sitoendelea kuwa kocha mkuu wa Ufilipino,” imeeleza taarifa ya kocha huyo iliyowasilishwa katika vyombo vya habari vya ufilipino.

“Ninajua nitawakwaza wengi lakini ukweli ni kwamba nimefikia maamuzi haya bila kushurutishwa na yoyote, na wala sijagombana na yoyote katika chama cha soka nchini Ufilipino, nimetafakari na nimeona kuna haja ya kujiondoa katika kazi hii.”

Scott Cooper, ambaye aliteuliwa kuwa msaidizi wa Butcher, tayari ameshatajwa kuchukua nafasi ya kocha huyo kutoka nchini England, na kazi kubwa itakayomkabili ni kukiandaa vyema kikosi cha Ufilipino kabla ya kwenda kushiriki fainali za barani Asia.

Kikosi cha timu ya taifa hilo kinatarajiwa kuweka kambi nchini Bahrain mwezi Septemba mwaka huu, kabla ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki na timu ya taifa ya nchi hiyo.

Meneja wa timu ya taifa ya Ufilipino Dan Palami, amesema wanaheshimu maamuzi yaliyochukuliwa na kocha Butcher, na wamempa baraka zote za kuondoka nchini humo, baada ya kuamua kuvunja mkataba wake.

“Nikiwa kama meneja wa timu ya taifa, tumepokea taarifa za Butcher kwa masikitiko makubwa, lakini hatuna budi kuheshimu alichokiamua na kuangalia mbele kwa ajili ya ushiriki wa timu yetu,” alisema kiongozi huyo kuviambia vyombo vya habari nchini humo.

“Ni kama bahati mbaya, lakini haitokua mara ya kwanza kwa kocha kutangaza kujiuzulu nafasi yake, wapo wengi waliowahi kufanya hivyo na timu walizoziacha zilifanya vizuri, ninaamini hata Ufilipino itakwenda kwenye fainali za Asia na itafanya vizuri.”

Timu ya taifa ya Ufilipino imepangwa kundi moja na Korea Kusini, China a Kyrgyzstan katika fainali hizo ambazo zitaanza rasmi Januari 05 na kumalizika Februari Mosi.

Apple yawa kampuni ya kwanza kufikia thamani ya $1 trilioni
Kampuni 10 zatangaza nafasi za kazi