Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Shakhtar Donetsk ya nchini Ukraine Mateus Cardoso Lemos Martins “Tete” amekiri na kuwa na ndoto za kuihama klabu hiyo, na kujiunga na moja ya klabu tatu kubwa barani Ulaya.
Tete raia wa Brazil, ameweka hadharani matarajio yake ya kuondoka Ukraine alipohojiwa na jarida la michezo la Esporte Interativwa, katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya maambuki ya virusi vya Corona, yanayoendelea duniani kote.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20, amesema klabu anazotamani kuzitumikia maisha mwake baada ya kuondoka Shakhtar Donetsk ni FC Barcelona (Hispania), Manchester United na Liverpool zote za England.
“Klabu tatu ambazo ni sehemu ya ndoto yangu hapa Ulaya ni FC Barcelona, Manchester United na Liverpool. Ni klabu kubwa zenye mameneja wazuri na idadi kubwa ya mataji. Kama mchezaji, ndoto yangu ni kushinda mataji muhimu na klabu hizo ni uchaguzi mzuri wa kufanikisha hilo, ” Aliliambia jarida la Esporte Interativwa
“Ninajua Manchester United na Liverpool ni wapinzani. Lakini, ikiwa wakati wa kuchagua, nitalazimika kufanya maamuzi ya busara, hasa kwa klabu itakayokua tayari kuhitaji huduma yangu.”
Licha ya kutaja FC Barcelona mchezaji huyo aliyekuzwa na kulelewa kisoka na klabu ya Grêmio ya nchini kwao Brazil, anaamini mtindo wake wa uchezaji ungefaa zaidi kwa kucheza Ligi Kuu ya England.
“Ligi ya England (EPL) ni mashindano ya kushangaza, mchezo unachezwa kwa kasi kubwa, kuna mameneja wengi na vilabu vikubwa,” Ninahisi wachezaji wana uhuru zaidi wa ubunifu hapo. Hiyo ndiyo tofauti kati ya ligi hiyo na ligi nyingine za Ulaya. “
Tete alisajiliwa na Shakhtar Donetsk mwaka 2019 na ameshaifungia klabu hiyo mabao matano katika michezo 24 aliyocheza. Pia amekua akiitwa kwenye kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 cha Brazil na tayari ameshacheza michezo saba.