Takriban watu 100 wamepoteza maisha baada ya tetemeko la ardhi kutikisa kisiwa cha Lombok nchini Indonesa, jana.
Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa kisiwa hicho kiligubikwa na kelele za watu waliohitaji msaada huku majengo yakianguka, umeme ukikosekana pamoja na kupotea kwa miundombinu yote ya mawasiliano kwa njia ya simu.
Boti za uokoaji zilifika katika kisiwa hicho na kufanikiwa kuwaokoa watalii zaidi ya 1,000 walikuwa kwenye kisiwa cha jirani cha Gili.
Mashirika ya msaada yameeleza kuwa yalitoa msaada wa chakula na malazi kwa wakaazi wa eneo hilo ambao baada ya kukimbilia maeneo mengine hawakutaka tena kurejea kwenye nyumba zao kwa hofu ya kupoteza maisha. Mashirika hayo ya misaada yamesema kuwa tetemeko la jana lilikuwa kubwa zaidi ya lile la wiki moja iliyopita ambalo lilisababisha vifo vya watu 16.
Rais wa Indonesia, Joko Widodo ametaka mamlaka za uokoaji kuongeza jitihada za mapema za kuwaondoa watu waliojeruhiwa huku akitaka ndege nyingi zaidi zitumwe maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uokoaji na kuwasafirisha watu walionusurika.
Msemaji wa wa Idara ya Udhibiti wa Majanga, Sutopo Purwo Nugroho amesema kuwa eneo la kaskazini mwa Lombok ndilo lililoathiriwa zaidi na tetemeko hilo. Imeelezwa kuwa takribani 80% ya eneo hilo imeharibiwa.
Serikali imesema watu 236 wamejeruhiwa na kwamba huenda idadi ya vifo vitokanavyo na tetemeko hilo ikaongezeka.