Tetemeko kubwa la ardhi limeikumba nchi ya Mexico wiki hii na kusababisha vifo vya watu takribani 248 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mexico City.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya nchi hiyo, tetemeko hilo limeangusha majengo marefu na nyumba za kawaida na kwamba maelfu wamelazimika kuhama makazi yao.

Rais Enrique Peña Nieto, katika tamko lake kwa umma ameeleza kuwa watoto 20 wamepoteza maisha na wengine 30 hawafahamiki walipo baada ya tetemeko kuangusha jengo la shule waliyokuwa wanasoma.

Tetemeko hili linatajwa kuwa na madhara makubwa zaidi katika kipindi cha miaka 32 iliyopita, baada ya tetemeko lingine lililochukua uhai wa maelfu ya wananchi.

Imeripotiwa kuwa zaidi ya watu milioni mbili katika jiji hilo wamekosa huduma za umeme na mawasiliano ya simu.

Serikali imeonya watu kutovuta sigara wakiwa mitaani ili kuepuka hatari inayoweza kutokana na kupasuka kwa mabomba ya mafuta na gesi.

Tetemeko hilo pia limetishia nchi jirani na taifa hilo ambazo zimetahadharishwa kuchukua hatua mapema.

 

 

UNHCR yaitaka Congo-DRC kuimarisha ulinzi kwa wakimbizi
Trump, Netanyahu waungana kuzishambulia Korea Kaskazini na Iran