Maafisa wa Chama tawala cha Taliban, wamesema tetemeko kubwa la ardhi limeua takriban watu 1,000 na kujeruhi wengine 1,500 katika maeneo ya mashariki mwa nchi ya Afghanistan.
Hatua hiyo, imepelekea Taliban kuomba msaada wa kimataifa kwa ajili ya juhudi za uokoaji huku picha zikionyesha maporomoko ya ardhi na kuharibu nyumba zilizojengwa kwa udongo katika jimbo la Paktika.
Tukio hilo, linadaiwa kutokea majira ya saa moja kamili ya usiku wa Juni 21, 2022 na inasadikika watu wengi walikuwa tayari wamelala huku mamia ya nyumba yakiharibiwa na tetemeko hilo la kipimo cha richa 6.1, lenye kina cha kilomita 51 sawa na maili 32.
Maafisa hao wamesema, tetemeko hilo la ardhi lilipiga takriban kilomita 44 kutoka mji wa Khost huku maeneo ya mbali kama Pakistan na India yakitajwa kupata msukosuko huo sawa na mji wa mkuu wa Afghanistan Kabul, na mji mkuu wa Pakistan Islamabad.
“Tunaomba Umoja wa Mataifa kutuunga mkono katika suala la kutathmini mahitaji na kujua namna ya kuwasaidia watu walioathirika ili kuweza kuwapa ahueni ya kilichowakumba,” walisema Viongozi hao.
Mwakilishi maalum wa Uingereza nchini Afghanistan, Nigel Casey, alisema nchi yake inawasiliana na Umoja wa Mataifa na iko tayari kuchangia mwitikio wa kimataifa ili kutoa msaada zaidi.
Naye Sam Mort kutoka kitengo cha UNICEF Kabul amesema matetemeko ya ardhi yanaelekea kusababisha uharibifu mkubwa nchini Afghanistan, kutokana na makazi mengi yaliyopo vijijini kutokuwa na utulivu au kujengwa vibaya.
Kwa upande wake Mkulima wa eneo hilo Alem Wafa aamesema timu rasmi za uokoaji bado hazijafika kijiji kimoja cha mbali cha Gyan, ambacho kina watu wengi zaidi walioathiriwa na tetemeko hilo.
“Hakuna wafanyakazi rasmi wa kutoa misaada, lakini watu kutoka miji na vijiji jirani walikuja hapa kuokoa watu na nilifika asubuhi ya leo, na mimi mwenyewe nieshuhudia miili ya watu 40.
Hili linatajwa kuwa ni tetemeko baya zaidi kuwahi kuikumba Afghanistan katika miongo miwili, huku Afghanistan ikiwa na vuguvugu la vita ya sheria za Kiislamu, ambalo lilipata mamlaka tena 2021 baada ya serikali inayoungwa mkono na nchi za Magharibi kuanguka.