Wakati wadau wa soka nchini wakisubiri kuthibitishwa kwa taarifa ya aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans Mwinyi Zahera kutua kwa mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, inaelezwa kuwa Mcongoman huyo huenda akapewa majukumu mazito huko Msimbazi.

Tetesi za Mwinyi Zahera kuwa sehemu ya Simba SC ziliibuliwa mwishoni mwa juma lililopita, huku ikielezwa kuwa kocha huyo ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Florent Ibenge kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa ya DR Congo atakuwa na kazi ya kuvumbua vipaji kwa ajili ya timu zote tatu (Vijana, Wanawake na Wakubwa).

Kazi hiyo ya kuvumbua vipaji itahusisha wachezaji wa ndani na nje ya Tanzania, lakini atapewa jukumu la kuisimamia timu ya vijana katika masuala ya kiufundi.

Zahera anatakiwa kuwa sehemu ya mikakati ya timu katika masuala ya kiufundi pamoja na maendeleo kwa kushauri au kutoa ambalo analifahamu.

Kuanzia sasa anatakiwa kuwa mshauri katika masuala ya usajili kwa wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia Simba kutokana na mapungufu ambayo wameyaonyesha awe mchezaji wa ndani au nje ya nchi.

Taarifa zinaenda mbali na kusema Zahera amekuwa akishauri masuala muhimu katika benchi la ufundi la Simba SC, ambalo lipo chini ya kocha Didier Gomes na amekuwa akiangalia masuala ya kimaendeleo ndani na nje ya timu.

Al Nabi kutua na kikosi kazi Young Africans
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 20, 2021