Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Mwadhama Protase Kadinali Rugambwa, kwa kusimikwa rasmi na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kuwa Kardinali.
Pongezi za Rais Samia zinakuja kufuatia Papa Francis kuwateua Makadinali wapya 21 katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petron jijini Vatican ambapo Papa aliwavisha makadinali hao kofia nyekundu, ambazo ni mahususi katika kuwatambua maafisa wapya wa kanisa hilo.
Hata hivyo, mmoja wa makadinali Luis Pascual Dri wa Argentina (95), hakuhudhuria hafla hiyo kutokana na chagamoto ya umri huku uteuzi wa baraza hilo, ambalo ndio huchagua mapapa wapya na huenda ukatoa nafasi kwa kiongozi huyo kuanzisha mchakato wa kumchagua mrithi wake.
Hatua hii mpya ina maanisha kuwa makadinali 99 kati ya 137 ambao kwa sasa wana uwezo wa kumchagua papa ajaye, wameteuliwa na Papa Francis mwenyewe, mwenye umri wa miaka 86.
Katika salam zake, Rais Dkt. Samia ameandika kuwa “Kauli mbiu ya utume wako ni “Enendeni ulimwenguni kote”, ikiakisi mafundisho ya Yesu Kristo katika Injili ya Marko 16:15, juu ya utume unaojali watu wote, sehemu zote na wakati wote. Naungana na Watanzania wote kukuombea kheri, afya njema, na mafanikio katika utumishi wako.”