Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ya binadamu na kuziondoa  kwenye soko pamoja na kusitisha matumizi yake kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya wakufunzi  wa ufuatiliaji juu ya ufundishaji na uhamasishaji  wa masuala ya udhibiti  wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa zisizo salama.

Amesema kuwa katika kudhibiti matumizi ya dawa zisizofaa TFDA imeondoa  dawa ya sindano aina ya Chloramphenical kwenye soko baada ya shirika la Afya Duniani WHO,  kubaini dawa hiyo ina  madhara kwa watumiaji, pia mamlaka hiyo imefuta usajili wa dawa  zingine kama vile Ketoconazole, (vidonge) Phenylpropanalamine, Dextropropoxyphene, Nimesulide,stavudine 40, Gatifloxacin, Rofecoxib, pamoja na Celecoxib baada ya kuthibitika zina madhara kwa watumiaji.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa TFDA amesema kuwa mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini kote na yanafanyika katika mikoa mbalimbali  yakiwashirikisha Madaktari, Manesi, na wafamasia  walioko kwenye  hospitali, vituo vya afya na Zahanati.

Hata hivyo, ameongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi wa masuala ya usalama wa dawa kutoka 73 hadi 133 na tayari katika kipindi cha miaka mitatu 2014/ 15 hadi 2017/18, Mamlaka ya chakula na dawa imehamasisha watendaji wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa uhamasishaji unaendelea  katika mkoa wa Katavi.

 

Albam mpya ya Chris Brown yaweka rekodi Billboard
Idadi ya waliofariki kwa mlipuko Kagera yaongezeka