Shirikisho La Soka Nchini Tanzania ‘TFF’ limethibitisha kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumamosi (Desemba 11), ambao utazikutanisha Simba SC na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Tayari TFF imeshamtangaza Mwamuzi Herry Sasii kusimamia sheria 17 za mchezo wa soka siku hiyo, huku ikiwahimiza Mashabiki kuendelea kukata tiketi zitakazowawezesha kuingia Uwanja wa Mkapa siku hiyo.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jumatano (Desemba 08), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya TFF Clifford Mario Ndimbo amesema maandalizi ya mchezo huo wa Watani wa Jadi yanaendelea vizuri hadi sasa.
“Maandalizi yanakwenda vizuri hadi sasa, tunaaamini timu zote zinaendelea kujiandaa kuelekea mchezo huu wa Jumamosi, na tunatarajia mchezo mzuri na wa kiungwana.”
“Tiketi zinaendelea kuuzwa katika vituo ambavyo vimeshatangazwa, tunawahimiza Mashabiki waendeleea kununua tiketi zao ili kufanikisha lengo la kufika Uwanja kushuhudia mchezo huu.”amesema Ndimbo.
Miamba ya Soka la Tanzania Simba SC na Young Africans inaelekea kwenye mchezo huo, huku zikiwa na tofauti ya alama mbili katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans inaongoza Msimamo huo ikiwa na alama 19, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 17.