Shirikisho la soka nchini TFF limetoa ufafanuzi wa zawadi Pesa kwa bingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ Simba SC, baada ya kuifunga Young Africans, Jumapili (Julai 25) Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
TFF imetoa ufafanuzi kufuatia Simba SC kukabidhiwa Kombe la Ubingwa bila pesa taslimu shilingi milioni 50, wakati wa shamra shamra za ubingwa, Uwanja wa Lake Tanganyika.
Rais wa TFF, Wallace Karia amesema suala la zawadi ya mshindi lipo chini ya Mkurugenzi wa Mashindano, Salum Madadi au katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao.
“Lini bingwa wa FA atakabidhiwa zawadi ya pesa hilo linashughulikiwa na mkurugenzi wa mashindano na katibu wao ndiyo wana ratiba ya jambo hilo,” amesema Karia.
“Ni mapema sana kuzungumzia hili, lakini tayari wamepata kombe na wakati wowote ule watakabidhiwa zawadi ya pesa taslimu shilingi milioni 50, ambazo hupewa bingwa wa FA,” amesema Mkurugenzi wa mashindano Salum Madadi.
Hata hivyo, hakueleza sababu za Simba SC kutokukabidhiwa mfano wa hundi sanjari na Kombe la Ubingwa, tofauti na ilivyokua mwaka 2020, Uwanja wa Nalson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.