Hali ya hatari imetangazwa kwa wadau wa soka wenye nia ovu ya kupanga matokeo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania 2019/20.
Shirikisho la soka nchini TFF kupitia Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), limesema litaongeza umakini kwenye michezo yote Ligi Kuu ili kuzuia matukio ya upangaji matokeo.
Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto, amesema wanaongeza uangalizi kwenye mechi zilizobaki za Ligi Kuu, ili kupatikana matokeo halali kutokana na timu nyingi kuwa katika hatari ya kushuka daraja, huku kila moja ikitaka kujinasua kwenye janga hilo.
“Uangalizi utaongezeka, tutaongeza wajumbe kwenye michezo yote ili matokeo yote yawe halali. Uchunguzi umeonyesha kunapokuwa na waangalizi, basi kunakuwa na uhakika zaidi wa matokeo halali,”alisema Mguto.
Mwenyekiti huo amesema michezo iliyobaki ni michache, hivyo wana uwezo kupeleka wajumbe nchi nzima, kwa sababu watapeleka pale tu ambapo wanaona mechi hiyo inaweza kuwa na matokeo chanya kwa timu zote.
Katika kile kinachoonekana kama kauli ya Mguto imeanza kufanyiwa kazi, kwenye michezo yote saba iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita, asilimia kubwa ya timu zilizokua mwenyeji hazikupata matokeo mazuri.
Young Africans ikiwa nyumbani Uwanja wa Taifa ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui, Biashara United nayo ikapata matokeo kama hayo Uwanja wa Karume mjini Musoma dhidi ya Coastal Union, na Kagera Sugar ikachezea kichapo cha 2-1 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba dhidi ya Polisi Tanzania.
Mtibwa Sugar ikiwa CCM Gairo, ikachapwa bao 1-0 dhidi ya KMC, Namungo, katika Uwanja wa Majaliwa mjini Lindi ikalazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons, Ndanda ikafungwa nyumbani Nangwanda Sijaona mjini Mtwara bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, na Ruvu Shooting ikiwa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani ikakubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya vibonde, Singida United.