Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ameitabiria ushindi klabu ya Simba katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kutokana na usajili wa klabu hiyo.
Amesema hakuna shaka timu hiyo ndiyo itakayochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2017/18.
Madadi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano ulioandaliwa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa jijini Dar es Salaam kuzungumzia ujio wa Klabu ya Everton ya England Julai 12, mwaka huu.
Madadi amesema jinsi Simba inavyoendelea na usajili wake ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu ujao.
“Simba itakuwa bingwa kwani inafanya usajili mzuri na kwa jinsi wanavyoenda ni wazi watakuwa na kikosi bora cha ushindani kwa msimu ujao wa ligi na mechi za kimataifa.
“Mabingwa wa msimu ujao Simba wanaweza kupata fursa ya kucheza na Everton pia mabingwa wetu watetezi Yanga, hii tunaomba kama itawezekana wacheze na Everton kabla ya Ligi ya England kuanza,” alisema Madadi.
Akizungumza kuhusu utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba kwa utani amesema; “Kwenye suala hili la ubingwa wa Simba msimu ujao, hebu tusubiri mwisho wa msimu tuone ila kwa kuwa amesema mkurugenzi wa ufundi haya.”