Shirikisho la soka nchini (TFF) limeweka wazi kuanza mchakato wa kumpata kocha mpya wa timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars) anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Salumu Mayanga ambaye mkataba wake umemalizika.
Kaimu katibu mkuu wa TFF Wilfrea Kidao, amesema wanachukulia kwa uzito mkubwa mchakato huo, ili kuhakikisha wanaajiri kocha mwenye uwezo na weledi wa hali ya juu kuinua kiwango cha mpira wa miguu hapa nchini.
“Tunataka tuajiri kocha wa national team kwa mchakato utakaokuwa huru, kwa hiyo anaweza kuwa Mayanga au mwingine au akatoka nje ya nchi, kuna makocha wengi wameshaleta CV, hili ni jambo kubwa linatakiwa umakini wa hali ya juu na ndiyo maana hatutaki kukurupuka,”.
“Kuna vitu vingi tunaangalia sio ubora wa kocha pekee, je kuna uwezo wa kumlipa huyo kocha mwenye kiwango hicho!? na ubora wa kocha huyo ni vitu ambavyo vinafanyiwa kazi”, amesema Kidao.
-
Ngorongoro Heroes waichapa Msumbiji
-
Welayta Dicha kuamua safari ya Young Africans
-
Uwanja wa Samara (Cosmos Arena) bado haujakamilika
Aidha, Kidao amesema wanatarajia kuwasilisha majina ya makocha nafasi ya kuifundisha timu hiyo kwenye kamati maalum itakayoundwa ili kukagua uwezo wa makocha hao kabla ya kuwasilisha majina kwa kamati ya utendaji ili kuanza mahojiano.
“Tunataka tuwe na kikosi kazi ambacho kitakuwa na wataalam waliobobea watusaidie kushortlist majina kwa ajili ya kupeleka kwenye kamati ya ufundi kwa mujibu wa katiba yetu, kamati ya ufundi ndiyo inapeleka mapendekezo kwenye kamati ya utendaji”, amesema Kidao.
Wakati huo huo,Kidao hakuacha kumpa sifa kocha Mayanga kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa timu hiyo licha ya kushindwa kufuzu mashindano makubwa ikiwemo Mataifa Afrika mwaka 2017 na kombe la Dunia litakalokwenda kufanyika mwezi Juni nchini Urusi.
“Mayanga ni kati ya walimu ambao wamekuwa na matokeo ya kuridhisha alituingiza kwenye nusu fainali ya COSAFA, kwa kocha mzawa tunapaswa kumsifu kwa matokeo ambayo ameonesha na tuna imani kocha atakayekuja atafanya kazi naye”, ameongeza Kidao.
Mayanga yuko nchini Algeria na timu ya Taifa ambapo wanajiandaa kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika hii leo nchini humo, kabla ya kucheza mchezo mwingine dhidi ya DRC Congo Machi 27, 2018 jijini Dar es Salaam.