Shirikisho la soka nchini TFF limethibitisha kufanya mabadiliko ya michuano ya ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20, ambayo hushirikisha timu za vijana za ligi kuu ya soka Tanzania bara, sambamba na kutambulisha michuano mipya ya vijana chini ya umri wa miaka 15 na 17.
Michuano hiyo ya vijana nchini inatarajiwa kufanyika kati ya Mwezi Oktoba 2018 – April 2019, huku msisitizo ukItolewa kwa timu shiriki kuhakikisha zinafanya usajili kwa wakati na kufuata utaratibu maalum.
Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Salum Madadi amesema, katika marekebisho ya kanuni msimu wa 2018-2019 vilabu vyote vya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili vitalazimika kuwa na timu za Vijana.
Madadi amesema timu za Ligi Kuu zinapaswa kuwa na timu za vijana chini ya miaka 20 (U-20) na chini ya miaka 17 (U-17), huku timu za Daraja la Kwanza na Daraja la Pili zikitakiwa kuwa na timu za vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17).
Michuano ya Ligi ya U20 itaanza Oktoba ikishirika timu za vijana (U-20) kwa vilabu vyote kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, huku Mashindano ya U17 yatakyoshirikisha timu 68 za vijana kutoka vilabu vya Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili yakitarajiwa kuanza Novemba, 2018.
Michuano ya U15 itashirikisha jumla ya timu 35 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambayo inatarajiwa kuchezwa mwezi Disemba, 2018.
Dirisha la Usajaili kwa Wachezaji wa U20 & U17 litafungwa Agosti 17, 2018. Kila klabu itaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 22 kwa timu za U-20 na wachezaji wasiozidi 22 kwa timu za U-17.
Hata hivyo TFF imeweka wazi mpango wa kukabiliana na udanganyifu ambao huenda ukajitokeza katika usajili wa timu hizo za vijana kwa kuwataka viongozi wa klabu husika kutumia nyaraka maalum, ambazo zitaambatanishwa kwenye usajili wa wachezjai wao.
Nyaraka za kuambatanishwa kwenye mfumo wa usajili ni:
(i) Cheti cha Kuzaliwa/Kitambulisho cha Uraia/Pasipoti ya kusafiria
(ii) Fomu ya kumaliza Shule ya Msingi – TSM9
(iii) Cheti Cha Daktari
(iv) Mkataba (makubaliano)
(v) Historia ya mchezaji (Players Passport)
(vi) Majina matatu yaliyopo kwenye kitambulisho/cheti
(vii) Picha (passport size)