Shirikisho la soka nchini TFF limesisitiza kuwa fedha za maendeleo zitakazoletwa na FIFA kiasi cha Dola 500,000 zitatumika kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kisoka kama ilivyoainishwa katika utaratibu wa kutolewa kwake.

TFF imetoa msisitizo huo kupitia kwa katibu mkuu Wilfred Kidao alipozungumza na wadau wa soka nchini kupitia vyombo vya habari, ambapo amesema, kiasi hicho cha fedha hakitokwenda kwenye vilabu, kama ilivyokua inaelezwa siku za karibuni.

Mtazamo wa fedha hizo kupelekwa kwenye vilabu vya ligi kuu na ligi nyingine, uliibuka kufuatia hali mbaya ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la maambukizi ya virusi vya Corona, ambalo pia limekua sababu ya kusimama kwa ligi na shughuli nyingine.

“Fedha hizi zinatolewa kupitia programu iitwayo ‘FIFA Forward 2’. Ni kama mkataba ambao FIFA inakuwa imeingia na kila nchi mwanachama wake juu ya matumizi ya fedha hizo na hazitakiwi kutumika nje ya hapo.

Ukienda kwenye ‘FIFA Forward 2’ kila mwanachama anapewa Dola 1 milioni  ni karibu Sh 2.3 bilioni za Tanzania. Huwa wanatoa Januari na Julai. Wanapotoa Januari wanatoa bila masharti lakini lazima uwe umekidhi vigezo vya ukaguzi.

Kwa Tanzania ni fedha zinaitwa ‘operational cost’ ni fedha za uendeshaji wa shughuli za kimpira. Programu za vijana, wanawake, mishahara ya makocha wa timu za taifa.Na kwa sababu ni makubaliano, hizo fedha zinatumika kwa mujibu wa yale makubaliano,” alisema Kidao.

Kidao alisema kuwa maeneo ambayo fedha hizo zitaelekezwa ni malipo kwa waamuzi, malipo ya mishahara kwa makocha wa timu za Taifa pamoja na malipo ya mishahara kwa watumishi wa TFF na shughuli nyingine za uendeshaji za shirikisho hilo.

Rais Shein: Corona haitazuia uchaguzi mkuu 2020
Mazingiza aomba ustahamilivu Simba SC