Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ limefanya mabadiliko ya mfumo wa kuwania Ngao ya Jamii, kwa kuanzisha Michuano rasmi itakayoshirikisha timu nne mwanzoni mwa msimu.
TFF imetangaza mabadiliko hayo kupitia taarifa maalum iliyotolewa na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kisha kusambazwa katika Mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwajuza Mashabiki na Wadau wa soka nchini kote.
Mfumo wa awali ulikuwa ni Mchezo Mmoja tu kama unavyofanyika nchi nyingi Duniani ukijulikana kwa majina tofauti, lakini kuanzia msimu ujao wa 2023/24, Ngao ya Jamii itawaniwa na timu nne.
“Kutakuwa na shindano maalum la ufunguzi wa Ligi (Ngao ya Jamii) litakaloshirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi na Timu Bingwa wa Kombe la Shirikisho.”
“Endapo Bingwa atakua miongoni mwa washindi wa nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, timu iliyoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi, itashiriki shindano hilo.” Imeeleza taarifa hiyo
Kuanzishwa kwa Michuano hiyo ya kuwania Ngao ya Jamii, Tanzania itakua na Michuano aina tano inayotambuliwa na Shirikisho la soka ‘TFF’ kuanzia msimu mpya wa 2023/24.
Michuano hiyo ni Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC PL), Ligi Daraja la Kwanza (Championship), Ligi Daraja la Pili (First League), Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, Mabingwa wa Mikoa (RCL) na Ngao ya Jamii.