Rasmi Dirisha la Usajili kwa ligi za soka Tanzania Bara limefunguliwa leo Jumamosi (Julai Mosi) huku kila klabu sasa ikiwashiwa taa ya kijani kutangaza mastaa wake wapya.

Kufunguliwa kwa dirisha hilo kutazitoa klabu mafichoni zikiwemo Simba SC, Young Africans na Azam FC ambazo zitaweka wazi nyota wao wapya kuelekea msimu ujao.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo ilisema dirisha hilo litazihusisha timu za Ligi Kuu Tanzania, Ligi ya Championship, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu soka ya wanawake.

Dirisha hilo ambalo limefunguliwa rasmi leo Jumamosi (Julai Mosi) litakuwa na siku 60 ambapo litafungwa rasmi Agosti 31.

Aidha, TFF imezitaka klabu kutumia dirisha hilo vizuri kuimarisha vikosi vyao ndani ya wakati wakidai hakutakuwa na muda wa nyongeza mara dirisha litakapofungwa.

TFF iliongeza kuwa dirisha dogo la usajili litafunguliwa Desemba 16, 2023 kisha kufungwa Januari 15, 2024.

Ni wazi ligi itaanza huku usajili ukiendelea kwani tetesi zinasema ligi inatarajiwa kuanza Agosti 12, mwaka huu.

Usajili 2023/24: KMC FC yaongeza Milioni 300
Jiandaeni kujikinga na maafa -Dkt. Yonazi