Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ lifurahishwa na kazi inayofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO), katika kuendeleza soka la wanawake nchini.
Katibu Mkuu wa TFF ametoa pongezi kwa Shirika hilo wakati akifunga mafunzo ya uongozi katika michezo kwa makocha wanawake 42 kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, kupitia Programu ya ‘Mpira Fursa’ inayoendeshwa na KTO, ambayo yanafanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam, yakiendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Kidau amesema, ili kuunga mkono jitihada hizo, mapema mwaka 2023 TFF itaendesha kwa gharama zake mafunzo ya aina tatu ya soka kwa wanawake hao ikiwemo ukocha/ualimu, uamuzi (referee), na usimamizi/uongozi, huku akietoa zawadi ya mipira miwili kwa kila mshiriki wa mafunzo hayo, baada kuwapongeza kutokana na nidhamu waliyoionyesha katika kipindi chote cha mafunzo..
Kwa upande wake mwakilishi wa kurugenzi ya elimu na mafunzo ya ufundi (TVET) katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi Fides Lubuva, amepongeza ushirikiano ulioonyeshwa na TFF katika kuendeleza programu hii ambayo ilianzishwa kwa ushirikiano baina ya KTO na TFF huku akiwataka makocha hao kuhakikisha FDCs inakuwa na timu imara ili ziweze kushiriki michuano hadi ngazi ya taifa na kutoa wachezaji bora watakaoliwakilisha taifa katika michuano mikubwa.
Programu ya Mpira Fursa inalenga kukuza na kuendeleza soka la wanawake na wasichana kwa kuandaa wanasoka bora wa kike wenye kujiamini na kujithamini, na kama njia ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi.
Programu hii inatekelezwa katika vyuo 54 vya mMaendeleo ya Wananchi kwa ufadhili wa Sida na MasterCard Foundation; na katika shule 108 za msingi kwa ufadhili wa taasisi ya Watoto ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Foundation.