Shirikisho la soka nchini TFF kupitia kamati yake ya uchaguzi imesitisha taratibu za kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba uliopangwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli amesema kwa kiasi kikubwa mchakato wa uchaguzi huo haujafuata taratibu zinazotakiwa.

Kuuli amesema kwamba miongoni mwa mapungufu hayo ni ada ya uanachama kwa ngazi ya Uenyekiti pamoja na Wajumbe kutofautiana, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya klabu pamoja na TFF.

Tayari kamati ya uchaguzi ya klabu ya SImba ilikua imeshatangaza orodha ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo.

Nafasi ya mwenyekiti ilikua inawaniwa na wanachama wawili ambao ni aliyewahi kuwa kiungo wa klabu hiyo Mtemi Ramadhani, na mwingine Swedi Nkwabi aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji wakati wa utawala wa Ismail Aden Rage.

Nafasi za Wajumbe wa Wanawake waliojitokeza ni Jasmin Badar Soud na Asha Ramadhani Baraka, wakati Wajumbe wa Bodi ni Hussein Kitta Mlinga, Iddi Noor Kajuna, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Mohammed Wandi, Suleiman Haroub Said, Abdallah Rashid Mgomba na Christopher Kabalika Mwansasu.

Wengine ni Alfred Martin Elia, Mwina Mohammed Kaduguda, Ally Suru, Said Tully, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakar Zebo, Omar Juma Mazola, Patrick Paul Rweyemamu na Suleiman Omar Suleiman.

Fomu zilirejeshwa Jumamosi makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam na uchaguzi umepangwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye mjini Dar es Salaam Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Boniphace Lihamwike.

Douglas Costa awaomba radhi mashabiki, wachezaji
Meddie Kagere awabwaga Mahundi, Mponda