Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limefanya ukaguzi wa viwanja vinavyotumika kwa kombe la Shirikisho na kuzuia viwanja vitatu kutumika kwa mechi zinazofuata za hatua ya raundi ya tatu.
Viwanja ambavyo havitaweza kutumika kwa raundi hiyo ya tatu ni pamoja na Uwanja wa Nachingwea unaotumiwa na Majimaji Rangers ambao watalazimika kwenda Ilulu Lindi kucheza mchezo wake na Mtibwa Sugar kwenye raundi hiyo.
Uwanja mwingine ni uwanja wa CCM Mkamba Morogoro unaotumiwa na timu ya Shupavu nao hautatumika kwa raundi hiyo na badala yake Shupavu watautumia Uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa mchezo wake na Azam FC.
Nayo timu ya Ihefu ya Mbarali haitatumia Uwanja wake kwa raundi ya tatu dhidi ya Yanga na badala yake mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya.