Rais wa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’, Gianni Infantino ameeleza furaha yake na kulipongeza Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ pamoja na Tanzania kwa ujumla kwa busara inayotumia katika kukuza maendeleo ya soka nchini.
Infantino ameeleza hayo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, huku pia akimpongeza Rais wa Shirikisho Afrika ‘CAF’, Patrice Motsepe kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya.
“Ilikuwa furaha kuwa Tanzania na kuzindua miradi ya maendeleo ya FIFA Kigamboni na Tanga.
Pongezi nyingi kwa Wallace Karia, Rais wa TFF na Patrice Motsepe, Rais wa CAF pamoja na jamii nzima ya mpira wa miguu katika nchi hii nzuri.
“Kila nchi duniani ambayo ni sehemu ya FIFA inapata fedha za kuwekeza kwenye maendeleo ya soka, lakini kuna baadhi ya nchi ambazo ni maalumu sana, na zinawekeza fedha wanazozipata kwa busara na mtazamo wa mbele na hakika Tanzania ni mojawapo,” alisisitiza Infantino katika chapisho lake hilo.
Aidha, Infantino ambaye alikuwa nchini kwa ajili ya uzinduzi wa michuano mipya ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam ljumaa iliyopita (Oktoba 20), alizipongeza timu za Simba na Al Ahly ya Misri kwa mchezo mzuri siku hiyo sambamba na mashabiki walioonesha hisia na morali kubwa katika mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
“Kuzinduliwa kwa ligi mpya ya soka ya Afrika (AFL) ilikuwa tukio la kipekee kwelikweli!
“Hongera Simba SC na Al Ahly kwa mchezo mzuri pamoja na waamuzi kwa ubora wa kuchezesha.