Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewashukuru watanzania wote, wapenzi, na wadau wa mpira wa miguu Tanzania waliojitokeza usiku saa 8 uwanja wa ndege wa JK Nyerere kumpokea mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani Mbwana Samatta.

Baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa JK Nyerere, Samatta alipokelewa na viongozi wa serikali, TFF, familia yake wakiwemo baba na mama yake mzazi na watanzania wengi walijitokeza kumlaki mchezaji huyo.

Mara baada ya mapokezi ya uwanja wa ndege, TFF ilimpeleka moja kwa moja kupumzika katika hoteli ya Serena iliyopo eneo la Posta jijini Dar es salaam, ambapo imemlipia gharama ya kukaa kwa siku mbili.

Akiwa hoteli ya Serena, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mama Juliana Yassoda alitoa salamu za pongezi kwa niaba ya Serikali, kisha mchezaji alipata nafasi ya kuongea na waandishi wa habari.

Kwa kuwa Jumanne, Januari 12 ni Sikukuu ya Mapinduzi, na Janauri 13 ni fainali ya kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar, siku ya Alhamisi Januari 14 TFF imeandaa dua maalumu ya kumpongeza Samatta itakayongozwa na viongozi wa dini mbalimbali katika uwanja wa Karume kuanzia saa 11 jioni.

Hata hivyo ratiba zingine za kumpongeza Mbwana Samatta zinazoweza kuandaliwa na wadau wengine zinaweza kuendelea ilimradi TFF ijulishwe mapema kwa ajili ya kuratibu uwepo wa mchezaji mwenyewe.

Wastara afunga ndoa na Mbunge
Yaya Toure: Mimi kuikosa Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika ni Aibu Kwa Afrika