Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka nchini, Wilfred Kidao amesema kuwa sakata la Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura, halijaanza hivi karibuni bali ni la muda mrefu na lilikuwa chini ya uchunguzi
Amesema kuwa suala hilo ambalo limepelekea kufungiwa kwa Wambura, limeanza muda mrefu na lilitokana na ripoti ya ukaguzi ambayo ilibaini mambo mengi yaliyomuhusisha Wambura.
”Jambo hili lilikuwa chini ya ukaguzi kwa muda mrefu na kamati ya ukaguzi ina magwiji kwelikweli imelifanyia kazi vizuri mpaka kufikia hatua ya kutoa maamuzi hayo yaliyofikiwa kwahiyo halijaanza juzi”, amesema Kidao.
Aidha, Wambura ambaye alichaguliwa kama makamu wa Rais kwenye uchaguzi mkuu wa TFF uliofanyika mwaka jana mjini Dodoma, amefungiwa kutojihusisha na soka maisha yake yote.
Hata hivyo Wambura alisema hukumu hiyo ya kufungiwa imetolewa bila yeye kuhojiwa kwa namna yoyote ile huku akiongeza kuwa tangu waingie madarakani na Rais Wallace Karia hajawahi kuachiwa ofisi kama makamu ila mara zote Karia akisafiri alikuwa anaacha ofisi chini ya kidao.