Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’, limezikumbusha klabu zote nchini ambazo zimesajili wachezaji wa kigeni kutoka nje ya Tanzania kuhakikisha zinawalipia vibali vya kufanya na kuishi kihalali nchini.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo klabu ambazo hazitokamilisha zoezi hilo wachezaji wao hawatoruhisiwa kucheza ligi.
Msemaji huyo amesema wameamua kutoa angalizo mapema ili watakapofanya ukaguzi na kubaini wachezaji ambao hawajalipiwa kutakuwa na adhabu mbili ikiwemo Penati kwa usumbufu.
Ndimbo amesema agizo hilo linazihusu pia timu za Ligi ya Champioship, Daraja la Kwanza, Ligi Kuu na Ligi Kuu ya Wanawake.
Klabu ambazo zina wageni wengi ni Young Africans, Simba SC na Azam FC ambazo zinatarajia kutimiza idadi ya wachezaji 12 wa kigeni ambao watahitaji vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini.
Tangu kufunguliwa kwa dirisha hilo Young Africans imetambulisha wachezaji watatu wa kigeni ambao ni Max Zengeli Mpia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Gift Fred kutoka Uganda na Yao Attoula kutoka Ivory Coast.
Huku Simba SC ikiwatambulisha Willy Onana, Che Malone wote kutoka Cameroon, Fabrice Ngoma kutoka DRC na Aubin Kramo kutoka Ivory Coast. Azam FC wakiwatambukusha Djibril Syllah, Alassane Diao na Tidiane Sidibe wote kutoka Senegal.