Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) wanashirikiana katika mambo mbalimbali yanayohusu soka, ikiwemo uteuzi wa wachezaji wanaounda Timu za Taifa.
Mhe. Mwinjuma amesema hayo leo Alhamis (Novemba 2, 2023) Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu Swali la Mhe. Mwanakhamisi Kassim Said wa Jimbo la Magomeni aliyeuliza, TFF inashirikianaje na ZFF kupandisha hadhi Ligi ya Zanzibar.
“TFF imekua ikishirikiana na ZFF katika uteuzi wa wachezaji kwa Timu za Taifa za vijana, ambapo vijana kutoka Zanzibar wamekuwa wakiitwa katika timu hizo na hatimaye kucheza Timu ya Taifa ya wakubwa” amesema Mhe. Mwinjuma.
Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma amesema Shirikisho la Soka Tanzania chini ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekua ikishirikiana na ZFF katika Mipango mbalimbali na kubainisha kuwa hivi karibuni kutakua na Mafunzo ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi ya Zanzibar ambayo itajikita katika Menejimenti, uwekezaji, Udhamini na Masoko ili kuendeleza soka katika pande mbili za Muungano.