Katika harakati za kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuhamasisha utalii hapa nchini, wakala wa misitu Tanzania – TFS kwa kushirikiana na wadau wa utalii wameandaa michezo maalumu, ili kuhamasisha utalii wa ndani Mkoani Kagera.
Akizungumza baada ya ugawaji wa medali kwa washindi wa mashindano ya kukimbia yaliyofanyika katika msitu wa Rubale, Kamanda Msaidizi TFS kanda ya ziwa, Thomas Moshi ameeleza lengo la kuandaa mashindano hayo kuwa ni kuunga mkono jitihada za Rais.
Kamanda msaidizi – TFS, Thomas Moshi.
Amesema “sisi TFS tumeshiriki mashindano haya ikiwa ni juhudi za kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake ya Royal Tour kuhamasisha utalii na vivutio vilivyoko katika nchi ya Tanzania.”
Kwa upande wake afisa utalii bodi ya utalii ofisi za kanda ya ziwa, Rhoda Kabalua amesisitiza watu kujitokeza kwa njia ya michezo kuhamasisha utalii kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kutimiza malengo ya bodi ya utalii nchini.
Baadhi ya washiriki wa mbio za kuhamasisha utalii wakikimbia kwenye msitu wa Rubale.
Amesema, “nipende kutoa wito kwa watanzania wote waweze kushiriki kwenye hii michezo au mbio na waweze kufanya utalii wa ndani, Tanzania tunao utalii mkubwa na tumebarikiwa sana maeneo tofauti tofauti ya vivutio kuanzia hifadhi za taifa, maeneo ya historia na tamaduni nk.”
Awali, Muandaaji wa Rubale Forest Try Running na Mkurugenzi wa Victoria Event Organizer, Nelson Machibya amesema, “dhumuni kubwa la forest run ni kuhamasisha utalii hasa kanda ya ziwa.”
Washiriki wa mbio za kuhamasisha utalii wakiwa eneo la maporomoko ya maji msitu wa Rubale.
Ameongeza kuwa, “tukianza na mkoa wa Kagera ambayo imekuwa mbio maalum ya kukimbia katika vivutio vya utalii wa Rubale Forest ambao ni msitu wenye maporomoko ya maji, leo tumeweza kufanikisha kuweza kukimbia watu 100 ndani ya msitu wa Rubale tukiwa tumepita katika vivutio mbalimbali.”