Mwandishi wa Habari na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu ushiriki wa klabu ya Simba SC kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC msimu huu 2021/22 ilianzia mzunguuko wa pili huku Young Africans ikipangwa kuanza Mzunguuko wa kwanza dhidi ya Rivers United ya Nigeria na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Simba SC ilicheza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana iliyopita kwa faida ya bao la ugenini, kwa kuwafunga Mabingwa hao wa Tanzania mabao 3-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wakitangulia kufungwa nyumbani kwao Gaberone mabao 2-0.
kufuatia kauli tata zilizochukua nafasi miongoni mwa wadau wa soka la Bongo jana Jumanne (April 19), baada ya Msemaji wa Young Africans Haji Manara kuzungumza na Waandishi wa habari na kusema Young Africans ndiyo klabu pekee itakayoanzia Mzunguuko wa Pili msimu ujao.
Thabit ametoa ufafanuzi huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa kuandika: Msimu huu wa mashindano ya CAF, Simba ya Tanzania ilianzia raundi ya pili ya mchujo.
Siyo kwa sababu walikuwa mabingwa wa Tanzania, hapana. Hakuna bingwa wa ligi yoyote anayeanzia raundi ya pili ya mchujo.
Simba walianzia raundi hiyo kwa sababu ya mafanikio yao kwenye mashindano ya Afrika kwa miaka mitano iliyopita.
Robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa ziliwafanya wajikusanyie alama 24 na kupanda kwenye viwango vya CAF.
Hadi ratiba ya 2021/22 inapangwa, Simba ilikuwa nafasi ya 15 Afrika kwa viwango vya ubora vya CAF ???!
Lakini hata hivyo, kwa nafasi hiyo, bado walikuwa hawastahili kuanzia raundi ya pili ya mchujo.
Kwa kawaida, vilabu vinavyoshika nafasi 10 za juu kwa ubora ndiyo huanzia raundi ya pili.
Simba walifaidika na kushindwa kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa RS Berkane ya Morocco ambayo ni ya nane.
Nafasi yake ilitakiwa ichukiliwe na aidha Pyramids (11) ya Misri, JS Kabylie (12) ya Algeria na hata AS Vita (13) ya DRC au Kaizer Chiefs (14) ya Afrika Kusini, lakini wote hawa hawakufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa kwenye nchi zao.
Hivyo Simba aliyekuwa wa 15, ndiyo akapata nafasi hiyo. “Man Jadda Wa Jadda”.
MSIMU UJAO
Simba watakuwa nafasi ya 12 kutokana na robo fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo wamefika msimu huu.
Alama zao zimeongezeka hadi kuwa 28, na kama watafika nusu fainali wanaweza kujiongezea alama zaidi na kupanda juu zaidi.
Na kama itakuwa hivyo, wanaweza kuingia 10 bora na kupata moja kwa moja haki ya kuanzia raundi ya pili ya mchujo.
Lakini kama watatolewa na Orlando Pirates, basi watabaki katika nafasi ya 12 na kuomba zali kama la msimu huu…yaani wa juu yake wasifuzu ligi ya Mabingwa.
Na hao ni Pyramids wa Misri na RS Berkane ambao nchi mwao ni ngumu sana kupata nafasi ya ligi ya mabingwa kwa sababu ya ushindani.
Pyramids wana kikwazo cha wale miamba wawili wa Cairo, Al Ahly na Zamalek; na RS Berkane pia wana kikwazo cha miamba wawili wa Casablanca, Raja na Wydad.
Kwa hiyo Simba wanayo nafasi nzuri zaidi ya kuanzia. raundi ya pili kuliko sisi wengine wa KAWAIDA!?
Sisi kuanzia raundi ya pili ya mchujo bado sana. Ni hadi tuingie 10 bora ya viwango vya CAF!
Anyway, Mwenyezi Mungu ni wa wote!
-Zakazi,. Msemaji Azam FC