Kiungo Kutoka nchini Uganda na klabu ya Simba SC Thadeo Lwanga amesema yupo FIT kurudi Uwanjani baada ya kukosekana kwa siku kadhaa.
Lwanga amekua na bahati mbaya msimu huu, kufuatia kukosa utimamu wa mwili ‘FIT’ sambamba na kupata majeraha, hatua mbayo imemkosesha kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kwa michezo mingi tofauti na msimu uliopita.
Kiungo huyo amezungumza na Mashabiki wa Simba SC kupitia Simba APP, ambapo amethibitisha kwa sasa yupo tayari kurudi Uwanjani, kufuatia kupona kabisa majeraha yaliyomuweka nje kwa siku kadhaa.
Amesema jukumu kubwa lipo kwa Kocha Mkuu Franco Pablo Martin kumpa nafasi kwenye kikosi chake kesho Jumamosi katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Pamba FC.
“Mimi afya yangu inaendelea vizuri na niko fiti kwa sasa, kama mwalimu ataona inafaa anaweza kunipanga Jumamosi”
“Kikubwa nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani Jumamosi ili kutupa sapoti na tunaamini tutafanya vizuri.” amesema Lwanga
Simba SC ambayo ni Bingwa Mtetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ itacheza dhidi ya Pamba FC huku ikiwa na lengo la kuendelea kutetea ubingwa wake kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya kuumiliki kwa misimu miwili mfululizo.
Msimu wa 2019/20 Simba SC ilitwaa ubingwa wa Michuano hiyo kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-1, Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa, na msimu wa 2020/21 ilifanya hivyo kwa kuifunga Young Africans 1-0, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.