Wakati taarifa zikieleza kuwa, kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama (MWAMBA WA LUSAKA) anawaniwa na Young Africans, uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Simba SC umeripotiwa kufikia makubaliano na wakala wa mchezaji huyo.
Chama amekua kwenye tetesi za kuondoka Msimbazi kufuatia mkataba wake wa sasa kusaliwa na muda wa miezi minane, kabla ya kufikia tamati.
Taarifa zinasema kuwa uongozi wa Simba SC ulikua kwenye mazungumzo na wakala wa Chama na umekubali kumuongezea mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea timu hiyo kwa dau la milioni 180 na mshahara wa milioni 15 kwa mwezi.
Hata hivyo wakala huyo amewaambia viongozi wa Simba SC kuwa, ili mchezaji wake akamilishe taratibu za kusaini mkataba mpya, wanapaswa kuingiza kipengele cha kumruhusiwa kuondoka muda wowote iwapo atapata ofa nzuri zaidi nje ya nchi.
Kwa upande wa Simba SC nao wameweka sharti la kuingiz kipengele cha kumuuza kiungo huyo kwa dau la shilingi bilioni 2, endapo klabu yoyote itaonyesha nia ya kumsajili akiwa ndani ya mkataba wake.
Awali taarifa ambazo hazikua rasmi zilieleza kuwa, Chama aligoma kusaini mkataba mpya ndani ya Simba SC, huku Young Africans inyodhaminiwa na kampuni ya GSM ikihusishwa na mpango wa kumsajili kwa dau la shilingi milioni 300 na mshahara wa shilingi milioni 18 kwa mwezi.