Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Ally Kamwe amesema mpango wa klabu hiyo kuagana na baadhi ya Wafanyakazi wake maarufu kama ‘THANK YOU’ bado haujafika mwisho.
Kamwe ametoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jumatatu (Julai 02) jijini Dar es salaam, katika mkutano maalum ulioweka wazi mipango ya Young Africans kuelekea msimu wa 2023/24.
Ally Kamwe amesema: “THANK YOU bado hazijafika mwisho bado zinaendelea, wapo Wachezaji baadhi na Watendaji kwenye idara mbalimbali ambao ndani ya wiki hii watapewa THANK YOU na kuwafungulia fursa wakapate changamoto kwenye maeneo mengine”
“Mpaka sasa hivi kwa 100% usajili wa Young Africans umeshafungwa, Wachezaji wote ambao tulikuwa tunawahitaji tayari wameshasaini, tumefunga zoezi la usajili kinachofuatia ni kuwatambulisha Wachezaji hawa, tunasubiri tumalize zoezi la utambulisho wa jezi limalizike”
“Maana yake Wiki hii pia haiyofika mwisho tutaanza kushusha vyuma mmoja baada ya mwingine, ni vyuma kwelikweli, nimewaambia kuhusu jezi namba sita na wote mmeshindwa kumjua atakayevaa jezi namba 6, huyu ni mmoja kati ya wale ambao wameongezwa na mabalaa yao ni mabalaa mazito kwelikweli”
Katika hatua nyingine Ally Kamwe amesema kikosi chao kinatarajia kwenda nchini Malawi, kufuatia mwaliko maalumu kutoka kwa Serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kucheza mchezo maalumu kwenye maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru Julai 6, 2023.
“Tumepokea mwaliko maalumu kutoka kwa Serikali ya Malawi kucheza mchezo maalumu kwenye maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru wa Malawi itakayofanyika Julai 6, 2023. Ni heshima kubwa sana kwa Klabu yetu na kwa Taifa kwa ujumla”
“Mgeni wa heshima kwenye sikukuu za uhuru wa Malawi ni Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali ya Malawi ikatupa heshima hii ya kipekee kwa mualiko huu mkubwa na wa kihistoria”
“Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa wachezaji wetu ambao watatoka mapumzikoni na kuungana nasi kwenda kuiwakilisha Nchi na Klabu yetu kwenye mualiko huu mkubwa. Tunatarajia kuondoka siku ya Jumatano na kama kawaida yetu ndege maalum kabisa itatupeleka Malawi na kutusubiri kisha tutarejea Dar es salaam siku ya Alhamisi baada ya sherehe hizo” amesema Kamwe