Hatimaye Ripoti ya Benchi la Ufundi la Singida Fountain Gate, zamani Singida Big Stars imewafikia viongozi wa klabu hiyo, ambao watalazimika kuipitia kabla ya kuchukua maamuzi ya kiufundi.
Singida Fountain Gate ambayo itashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2023/24, itaitumia Ripoti hiyo kama Dira ya kufanya maboresho katika kikosi chao, ambacho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kinafanya vizuri katika michuano ya ndani na hiyo ya Kimataifa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Singida Fountain Gate Hussein Masanza amesema licha ya Ripoti hiyo kuwafikia viongozi, kwa sasa wachezaji wamepewa likizo baada ya ligi kufika mwisho huku wakitarajiwa kurejea hivi karibuni kwa maandalizi ya kambi ya msimu wa 2023/24.
Masanza amesema kuwa tayari ripoti kutokaa kwenye Benchi la Ufundi lililokuwa linaongozwa na Hans Pluijm imewasilisha ripoti hiyo, huku likiwa na matumaini makubw aya kutimiziwa kila kitu walichoainisha.
“Ripoti ya Benchi la Ufundi ambayo hiyo itatoa dira ya nini kifanyike kwenye maboresho ya kikosi chetu tayari ipo mezani kwa bodi.
“Ikiwa tayari Imeshawasilishwa kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza kufanyiwa kazi kwani bodi ikishapitia kazi inayobaki ni kufuata mapendekezo kwa kuwa benchi la ufundi linatambua kipi kinapaswa kufanyiwa kazi,” amesema Masanza.