Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora imeiomba Serikali na wadau mbalimbali kuandaa programu maalum za kuwasaidia wanawake hasa wa vijijini kutumia teknolojia katika kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya usawa wa kijinsia.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu katika Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke wa Afrika, na kuwataka Wanawake kuendelea kujiamini na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema, “siku hii muhimu pia inatukumbusha jukumu walilonalo wanawake wa kiafrika ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa ndani kama wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara, wanasayansi, na viongozi katika sekta nyingine nyingi.”
Jaji mwaimu ameongeza kuwa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaungana na jamii na wadau mbalimbali katika kutambua mchango wa Wanawake wa Afrika, na kwamba wataendelea kuwaenzi waanzilishi wa Umoja huo kwa ushujaa wao, ambapo umechangia kuhamasisha haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika ajenda ya ukombozi wa Afrika.