Kiungo wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani Bayern Munich Thiago Alcantara amefunguka na kueleza dhamira ya kutaka Kurudi FC Barcelona.
Alcantara ameeleza hadharani dhamira hiyo, ikiwa ni siku chache zimepita, ambapo Rais wa FC Barcelona Josep Maria Bartomeu alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza mpango wa kutaka kumrejea kiungo huyo klabuni hapo.
Jarida la michezo la Don Balon limefanya mazungumzo na Alcantara na kupata ukweli wa dhamira ya mchezaji huyo, ambaye alisajiliwa na Pep Guardiola kwenye klabu ya FC Bayern Munich akitokea FC Barcelona miaka minne iliyopita.
Alcantara bado ana mkataba na FC Bayern Munich hadi mwaka 2019.
Hata hivyo suala hilo la mkataba haliwezi kuwa kikwazo kwa FC Barcelona kumrejesha mchezaji huyo, endapo meneja mpya atakaebeba majukumu ya Luis Enrique atathibitisha kumuhitaji kwa ajili ya msimu ujao.