Kiungo kutoka nchini Hispania na Klabu ya Liverpool ya England Thiago Alcantara atakosa sehemu ya msimu huu 2022/23 iliyosalia baada ya kufanyiwa upasuaji.
Alcantara amefanyiwa upasuaji huo baada ya kuwa na tatizo kwenye paja lake kwa muda mrefu ambalo lilikuwa likimsumbua mara kwa mara.
Kiungo huyo alikosekana kwenye mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Tottenham na sasa ataikosa michezo inayofuata dhidi ya Fulham, Brentford, Leicester, Aston Villa na Southampton.
Awali Alcantara alipata tatizo hili dhidi ya Fulham kwenye mchezo wa Ligi Kuu akatupwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja.
Imeelezwa kuwa, ndiyo maana Liverpool wameamua kuchukua uamuzi wa kumfanyia upasuaji ili kuhakikisha mchezaji huyo anarudi akiwa imara zaidi.
Baada ya upasuaji ambao amefanyiwa, sasa inaelezwa kufika Julai mwaka huu kiungo huyo atakuwa fiti.
Kwa sasa Alcantara ataungana na Stefan Bajcetic kuwa nje ya uwanja mpaka msimu ujao.
Ikumbukwe kuwa, Liverpool inaendelea kupambana na sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Premier, huenda ikapenya ndani ya Top Four kwa mechi zilizosalia.