Beki kutoka chini Brazil Thiago Silva amekiri kuwa alimwomba Paulo Dybala ajiunge na Klabu ya Chelsea baada ya ripoti kuhusishwa na mshambuliaji huyo kuhamia Stamford Bridge.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia na Argentina, hivi karibuni amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Chelsea msimu huu wa majira ya joto, huku mchezaji huyo akiripotiwa kuwa na kipengele cha kuachiwa cha euro milioni 12 katika mkataba wake na klabu yake ya sasa ya AS Roma.
Akizungumza na Sky Sport Italia kuhusu tetesi hizo, nahodha wa Chelsea Thiago Silva alikiri kwamba alimuuliza Dybala kama anaweza kujiunga na The Blues hao, akisema: “Nilimwona Paulo Dybala hapa, (vyombo vya habari) vinazungumza juu yake kuja Chelsea. Nimezungumza naye na kumuuliza kama atakuja.
“Ni mchezaji wa kiwango cha kimataifa. Ningependa kucheza naye na utakuwa usajili mkubwa. Hebu tuone.”
Dybala alijiunga na Roma msimu uliopita baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Juventus, lakini amekuwa akiandamwa na majeraha tangu ahamie.
Wakati wa msimu wa 2022/23, fowadi huyo alikosa michezo 18 kutokana na majeruhi, lakini aliweza kufunga mabao 18 na kutoa pasi saba za mabao katika mashindano yote kwa kikosi cha Jose Mourinho ikiwa ni pamoja na moja kwenye fainali ya Ligi ya Europa.
Alipoulizwa na waaandishi wa habari wa Italia katika uwanja wa ndege Jumamosi, Kocha wa Roma, Mourinho kuhusu Dybala kwenda Chelsea alijibu: “Sijui kuhusu mkataba wake.”
“Lakini ni wazi nazungumza na Paulo kama ninavyofanya na wachezaji wangu wote.”
Chelsea tayari imekuwa hai katika dirisha la usajili la majira ya joto, ikiwasajili washambuliaji Christopher Nkunku na Nicolas Jackson kwa jumla ya euro milioni 87.