Mlinda mlango kutoka nchini Ubelgiji Chelsea Thibaut Courtois, jana jumatatu alishindwa kuripoti kwenye kambi ya mazoezi ya kikosi cha Chelsea (Cobham Training Centre), kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi ya England.
Mlinda mlango huyo alipaswa kuwasili kambini jana, baada ya kumaliza mapumziko, lakini mpaka mazoezi ya kikosi cha The Blues yanamalizika, kulikua hakuna hata dalili za kuwasili kwake katika uwanja wa maozezi huko magharibi mwa jijini London.
Meneja wa Chelsea Maurizio Sarri alikataa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu hatua ya kutokuwasili kwa mlinda mlango huyo, huku akiahidi kutoa ufafanuzi siku nyingine kuhusu mustakabali wa Courtois katika kikosi chake.
Vyombo vya habari vilifika katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea (Cobham Training Centre) kuthibitisha kurejea kwa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye amekua akiripotiwa kuwa katika harakati za kutaka kuihama The Blues, na kutimkia kwa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.
Mkataba wa Courtois na klabu ya Chelsea, unatarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu wa 2018/19, huku akikataa kusiani mkataba mpya kwa shinikizo la kutaka kuondoka katika kipindi hiki, ama kuondoka kama mchezaji huru itakapofika mwezi Julai mwaka 2019.
Wakati mlinda mlango huyo akishindwa kufika mazoezini hapo jana, klabu ya Chelsea ilithibitisha kuwasili kwa wachezaji wengine, baada ya kumaliza likozo za mapumziko na kuweka picha zao kwenye tovuti ya klabu hiyo. Wachezaji hao ni Eden Hazard, Ngolo Kante and Olivier Giroud.