Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Thierry Henry ameshindwa kusema lolote kuhusu mpango wa kufikiriwa kuwa mrithi wa meneja wa sasa wa klabu hiyo Arsene Wenger, ambaye huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu.
Wenger bado hajazungumza kuhusu mustakabali wake klabuni hapo, lakini mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa ma tetesi huenda akasaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja hadi miwili.
Gazeti la Daily Telegraph limeripoti kuwa, Henry amekua mmoja wa watu wanaopewa kipaumbele cha kukabidhiwa benchi la ufundi la Arsenal, na msimamo huo unashikiliwa na mtoto wa tajiri Stan Kroenke anaemiliki asilimia kubwa ya hisa za klabu ya Arsenal aitwae Josh.
Kwa sasa Henry anafanya kazi kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji sambamba na Roberto Martinez, ambaye alikabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo mwaka jana.
Henry aliwahi kuwa kocha wa kikosi cha vijana cha Arsenal, kabla ya kukorofishana na Arsene Wenger kufuatia kazi ya uchambuzi wa soka aliyokua akiifanya kwenye kituo cha televisheni cha Sky Sports, ambapo mara kadhaa alikuwa akieleza wazi wazi mapungufu ya klabu hiyo upande wa kikosi cha wakubwa.
Mshambuliaji huyo anaendelea kukumbukwa na mashabiki wa Arsenal kwa uwezo wake wa kucheza soka nafasi ya ushambuliaji, na wakati wa utawala wake alifanikiwa kufunga mabao 228.