Mabosi wa Simba SC wanaendelea kutajwa kuwa katika harakati nzito za kusuka kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, huku wakihusishwa na usajili wa Beki wa Timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Thierry Manzi ambaye amethibitishia kuwa wakati wowote atakuja Tanzania.

Beki huyo ambaye ni nahodha msaidizi wa Amavubi, amesema yupo njiani anakuja Tanzania kwa ajili ya kumalizana na Simba SC, baada ya taratibu za awali kufanywa na Uongozi wa Klabu hiyo, ambao umedhamiria kutimiza maagizo yaliyotolewa na Kocha Mkuu Robertinho.

Manzi aliyezipa mataji mbalimbali timu za APR na Rayon Sports za Rwanda kwa vipindi tofauti, hivi karibuni alikuwa Ubelgiji alikoenda kuzungumza na baadhi ya timu zilizotaka kumsajili, lakini sasa amebadili gia hewani na atarudi nchini kwao kisha kuja Tanzania kuzungumza na mabosi wa Simba SC.

“Kama kila kitu kitakuwa sawa nitakuja Tanzania kuzungumza na timu lakini kwa sasa nikitoka huku (Ubelgiji) nitaenda kwanza nyumbani Rwanda,” Amesema Manzi.

Beki huyo ni miongoni mwa wachezaji waliopendekezwa Simba SC na Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, anayeamini atamfaa kikosini hapo kwani waliwahi kufanya kazi pamoja miaka kadhaa nyuma wakiwa kikosi cha Rayon Sports kabla ya Robertinho kutimkia Gor Mahia ya Kenya na Manzi kwenda FC Dila ya Geogia, kisha FAR Rabat ya Morocco kabla hajavunja mkataba na kurejea AS Kigali ya Rwanda.

Aidha nyota mwingine aliyependekezwa na Robetinho ni winga Mcameroon Leandre Onana anayeongoza kwa ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Rwanda akifunga mara 15 akiwa na timu yake ya Rayon Sports sambamba na kuasisti mara sita.

Hata hivyo inafahamika kuwa Meneja wa Onana ndiye meneja wa Robertinho, hivyo huenda dili hilo likakamilika baada ya staa huyo wa Rayon kumaliza msimu kwa kucheza mchezo wa ligi dhidi ya Sunrise juzi Jumapili (Mei 28) na Fainali ya michuano ya ‘Peace Cup’ dhidi ya APR mapema mwezi ujao.

Hata hivyo, inaelezwa mabosi wa Simba SC nao wameshusha wachezaji wao katika maeneo tofauti na wale aliowapendekeza Robertinho na tayari wapo  Dar es Salaam wakisuburi makubaliano ya pande zote mbili ili wasaini mikataba.

Simba SC inataka kurejesha ufalme ilioupoteza kwa misimu miwili sasa na ili kuhakikisha hilo imepanga kusajili wachezaji bora ambao wataifikisha nchi ya ahadi.

Pia, tayari matajiri hao wa Msimbazi wameanza mazungumzo ya kuhakikisha inawabakiza mastaa wake muhimu kikosini na kuachana na wengine wengi ambao hawawahitaji.

Wachezaji kama kina Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Mohamed Ouattara, Ismail Sawadogo, Augustine Okrah na Peter Banda ni miongoni mwa wachezaji ambao huenda wakaondoka Simba mwishoni mwa msimu huu.

Rais akiri kutumia kilevi, awataja Polisi
Dodoma Jiji yatamba kuivurugia Namungo FC