Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema bado wana matumaini ya kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao, kutokana na michezo kadhaa iliyosalia.
Mtibwa Sugar imekua na mwenendo mbaya kwa msimu wa tatu mfululizo, hali ambayo imeifanya klabu hiyo kuwa miongoni mwa vilabu vinavyopewa nafasi ndogo ya kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao.
Akizungumza na Dar 24 Media Kifaru amesema, bado wana nafasi kubwa ya kupambana na kupata matokeo chanya yatakayowaweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu na kuwa miongoni mwa klabu zitakazosalia katika Daraja hilo.
“Bado tuna michezo sita iliyosalia kuhitimisha msimu wa ligi, miongoni mwa hiyo michezo tuna michezo mitatu tutakayocheza nyumbani katika Mashamba ya miwa na baadae kumalizia kwenye viwanja vya ugenini.”
“Tutacheza nyumbani dhidi ya Namungo FC, Ruvu Shooting na Azam FC, kisha tutatoka kwenda katika viwanja vya ugenini ambako tutacheza na Simba SC, Polisi Tanzania na tutamaliza msimu kwa kucheza na Young Africans.”
“Ninakiri hatuko mahala pazuri katika msimamo kwa sababu ukiangalia timu nyingi zina alama kuanzia 30 kurudi nyuma, ni jukumu letu kuhakikisha tunapambana ili kujiondoa katika hilo kundi na kubaki salama, Uongozi wa Mtibwa Sugar una matarajio makubwa sana ya kupambana na kubaki Ligi Kuu.” amesema Kifaru.
Baada ya sare ya bila kufungana jana Jumapili (Mei 15) dhidi ya Coastal Union, Mtibwa Sugar iliyokua nyumbani imefikisha alama 28 zinazoiweka kwenye nafasi ya 08 katika msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa.