Wakuu wa Idara za Habari na Mawasilino za klabu za Soka nchini wameombwa kuwa karibu na Vyombo vya Habari ili kutimiza wajibu na majukumu yao ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Habari Mwandamizi wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru alipozungumza na Dar24 Media, baada ya kuulizwa mapungufu anayoyaona kwa Wakuu wa Idara za Habari na Mawasiliano hususan klabu za Simba SC na Young Africans.
Kifaru amesema asilimia kubwa ya wakuu wa Idara hizo wameshindwa kutambua wajibu wao na kuheshimu mipaka ya kazi walizopewa kwenye taasisi, na mwishowe wanajikuta wametumbukia katika masuala binafsi.
“Wanashindwa kujitambua kwa sababu wanasahau misingi ya kazi zao, hawajui mipaka ya taasisi zilizowapa nafasi ya kuzisemea, ndio maana hawatoi ushirikiano kwa Wanahabari ili kuijuza jamii inayotaka kusikia nini kinachofanyika ama kitakachofanyika”
“Kwa mfano mimi ninawaheshimu sana Waandishi wa Habari, ndio maana ninakua mwepesi sana kutoa habari wakati wowote, sasa wengine utakua wakitafutwa wanatoa visingizio wapo kwenye mikutano, watafutwe baadae, halafu wakitafutwa hawataki kupokea simu ama wanaahirisha miadi ‘Apointment’ bila sababu,”
“Kwa hiyo niwakemee sana wasemaji wa klabu za Ligi Kuu na madaraja ya chini kwa kusema, hakuna jambo zuri kama kuwapa habari wanajamii wanaotaka kujua nini kinaendelea katika taasisi wanazozisemea, wafahamu wapo wanaotaka kufahamu na kupata habari kutoka kwao na sio za kuokota okota tu, na hii ndio inasababisha maneno mengi kwenye mitandao.” amesema Kifaru