Kiungo kutoka nchini Ghana Thomas Partey amewaambia viongozi wa Arsenal anataka kuondoka kwenye dirisha la Januari 2024, litakapofunguliwa.
Kiungo huyo mkabaji mwenye umri wa miaka 30, huu ni msimu wake wa nne akiwa na kikosi cha Arsenal baada ya kujiunga kwa ada ya Pauni 45 milioni akitokea Atletico Madrid.
Amefunga mabao matano katika mechi l04 na alikuwa na msaada mkubwa msimu uliopita wakati Arsenal ilipoonyesha nguvu kubwa kwenye mbio za ubingwa.
Lakini, kwa sasa taarifa zinafichua kwamba Partey anataka kwenda kuanza maisha mapya kwa kubadili timu dirisha la Januari 2024 litakapofunguliwa.
Kiungo huyo aliyecheza mechi 47 kwenye kikosi cha kimataifa cha Ghana nusura ashawishike na pesa za Saudi Arabia wakati klabu ya Al-Ahli ilipohitaji huduma yake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Na amekuwa akiwindwa pia na miamba ya Italia, Juventus.
Miamba hiyo ya Serie A ipo kwenye msako wa kiungo mkabaji na imepanga kufanya hilo kwenye dirisha la majira ya baridi na tayari mipango ya kumsajili Partey imeshaanza.
Partey mwenyewe yupo tayari kuhamia Turin, baada ya kupoteza namba kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal kufuatia ujio wa kiungo Declan Rice, aliyenaswa kwa ada ya Pauni l05 milioni kwenye dirisha lililopita.
Partey, ambaye mkataba wake huko Emirates utafika tamati mwaka 2025 anapiga hesabu pia kurudi kukipiga huko Hispania.