Meneja wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain Thomas Tuchel amekataa kuzungumzia suala la uwezekano wa kumsajili kiungo wa klabu ya Chelsea N’Golo Kante.
Kante, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa wa kombe la dunia Julai 15 baada ya kuifunga Croatia mabao manne kwa mawili, amekua katika harakati za kuwindwa na Paris Saint-Germain, huku msukumo wa usajili wa mchezaji huyo ukidaiwa kutolewa na Tuchel.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani, alikataa kuzungumzia suala hilo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari katika mkutano wa baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Atletico Madrid, na alijibu hayupo tayari kuzungumzia suala hilo.
‘Haipendezi kuzungumza jambo ambalo halihusiani na mkutano huu, sitaki kuingia katika malumbano na makocha wengine kwa sababu ya kutaja jina la mchezaji fulani,’ Alisema Tuchel.
‘Hivyo sina cha kusema kuhusu Kante, nipo hapa kwa ajili ya kuiandaa timu kwa msimu mpya wa ligi ya Ufaransa.’
Katika hatua nyingine imedaiwa kuwa mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe alikua mshawishi mkubwa wa kumtaka Kante akubali kurejea nchini Ufaransa na kuanzisha maisha mapya jijini Paris, ili afurahie ladha ya soka jijini humo.
Mbappe anadaiwa kufanya ushawishi huo wakati kikosi cha Ufaransa kilipokua nchini Urusi kwa ajili ya fainali za kombe la dunia zilizofikia tamati Julai 15.
Wakati huo huo Tuchel, aligoma kuzungumzia suala la uwezekano wa mshambuliaji wake kutoka nchini Uruguay Edinson Cavani, ambaye anahusishwa na taarifa za kutaka kuhamia kwa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.
Mshambuliaji huyo bado hajajiunga na kambi ya PSG, kufuatia kuwa na ruhusa ya mapumziko baada ya kumaliza majukumu ya kuituikia timu yake ya taifa kwenye fainali za kombe la dunia.
Cavani anahusishwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid kama mbadala wa mshambuliaji Cristiano Ronaldo, aliyetimkia kwa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus.
Thamani ya mshambuliaji huyo inatajwa kufikia Euro milioni 100 kama Real Madrid watathibitisha kuwa tayari kumsajili katika kipindi hiki.