Siku chache baada ya Shirikisho la soka Duniani FIFA kutangaza orodha ya wachezaji wanaowani tuzo ya Mchezaji Bora (Ballon d’Or), Meneja wa klabu ya Chelsea Thomas Tuchel, amejitokeza hadharani na kumpigia chepuo mchezaji wake Jorge Luiz Frello Filho ‘Jorginho‘.
Tuchel, amesema kiungo huyo mzaliwa wa Brazil anastahili kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu, lakini haamini endapo tuzo hiyo inatakiwa kuangaliwa kama muhimu sana.
Kiungo Jorginho sasa anawania tuzo nyingine binafsi baada ya kutajwa katika orodha ya wachezaji 30 waliotangazwa kuwania tuzo ya Ballon d’Or pamoja na Lionel Messi na Robert Lewandowski.
“Kwa uhakika Jorginho anastahili kushinda Ballon d’Or,” amesema Tuchel akinukuliwa na Bild.
“Hii ni tuzo binafsi, hata hivyo si kitu chenye thamani zaidi kwenye mpira wa miguu, na hatakiwi kukiwaza sana.”
“Lakini ningependa mchezaji ashinde, kwa sababu inaongeza kujiamini kwa mchezaji, lakini kwa upande wangu mimi si kitu muhimu sana.”
N’Golo Kante, Cesar Azpilicueta, Mason Mount na Romelu Lukaku pia wanaiwakilisha Chelsea kwenye orodha ya kuwania tuzo hiyo, na Tuchel anajisikia fahari zaidi kwa Lukaku, ambaye alirudi klabuni hapo Stamford Bridge akitokea kwa mabingwa wa Italia Inter Milan Agosti, mwaka huu.