Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich Thomas Tuchel amekutana na Mshambuliaji Harry Kane huko London kujadili uhamisho kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, imeelezwa.
Nahodha huyo wa England, Kane amebakiza miezi 12 tu kwenye mkataba wake wa sasa huko Tottenham Hotspur na amekuwa akivumishwa anaweza kupigwa bei kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Bayern walikuwa wa kwanza kupeleka ofa ya kumsajili Mshambuliaji huyo, walipoweka mezani Pauni 60.2 milioni, ambazo hata hivyo zilikataliwa na Spurs. Mabingwa hao wa Ujerumani watarudi Spurs na ofa mpya.
Kwa mujibu wa gazeti la BILD, kocha wa Bayern, Tuchel alimtembelea Kane kwake huko London kujadili uhamisho. Inaelezwa Kane anashawishika Bayern atakwenda kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kane anaishi kwenye jumba la Pauni 17 milioni akiwa na mkewe mrembo Katie na watoto wao watatu, Ivy, Vivienne Jane na Louis. Jumba hilo lina Gym na vyumba saba vya kulala.
Manchester United naye wamekuwa wakihusishwa na mshambuliaji huyo, lakini bado hawajapeleka ofa rasmi.
Chelsea, ambao kwa sasa wapo chini ya Kocha Mauricio Pochettino, aliyewahi kufanya kazi na mshambuliaji huyo huko Spurs, naye amekuwa akivutiwa na mpango wa kunasa saini yake.
Lakini, mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy hayupo tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa wapinzani wao wa ndani ya Ligi Kuu England, kitu ambacho kinaweza kuwapa unafuu Bayern wanaosaka straika mpya wa kwenda kuziba pengo la Robert Lewandowski.